Kesi ya jamaa aliyenaswa na bunduki eneo la Likoni imeahirishwa baada ya mshukiwa huyo kuugua.
Rama Ali Bamama alitiwa mbaroni wiki jana katika eneo la Mrima, Likoni akiwa na bunduki aina ya G3.
Bamama ameiambia mahakama hawezi kuendelea na kesi hiyo kutokana na maumivu ya meno aliyoyapata kutokana na kichapo alichopewa na polisi.
“Polisi walinipiga sana mpaka wakaniumiza meno. Siwezi kuendelea na kesi yangu mpaka nitibiwe,” alisema Bamama.
Hakimu mkuu Julius Nange’a, alikubali ombi la mshukiwa huyo na kuagiza apelekwe hospitali ili apate matibabu.
Mshukiwa huyo anadaiwa kuhusika katika visa vya wizi wa mabavu eneo la Likoni.
Aidha, anadaiwa kuwa mwanachama wa kundi la al-Shabaab aliyerudi nchini kutoka Somali.
Bunduki hiyo ilibiwa kutoka kwa afisa wa polisi wa Kituo cha Likoni ikiwa na risasi 20 lakini ilipatikana na risasi moja pekee.
Kesi hiyo itatajwa siku ya Alhamisi.