Kijana mmoja ametiwa mbaroni Jumampili katika eneo la Mutiambo, kata ya Ndalani kaunti ndogo ya Yatta kwa makosa ya kumchinja mbuzi wa mamake bila idhini.
Akidhibitisha kisa hicho, naibu was chifu wa eneo hilo Josphat Sila alisema kuwa kijana huyo amekuwa akimuhangaisha mama yake ambaye in mkongwe.
Sila alisema kuwa Jumamosi jioni kijana huyo alimchinja mbuzi wa pekee wa mamake bila idhini yake.
Aliongeza kuwa wiki iliyopita kijana huyo alichukua mwanambuzi wa mbuzi huyo na kumchinja.
"Mamake mshukiwa amekuwa akilalamika kusumbuliwa na mwanawe lakini mara nyingi nmekuwa nikiwashauri kutatua shida kama familia, ila kwa sasa maji yamezidi unga kwani Tabia za mshukiwa zinakera kila uchao," alisema Sila.
Baada ya kuhojiwa na maafisa was polisi kijana huyo alisema kuwa alifika nyumbani na kumpata mbwa wake akibweka kwa njaa ndipo akaamua kumchinja mbuzi wa mamake ili kujilisha pamoja na mbwa wake.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Matuu akisubiri kufikishwa kortini hapo siku ya Jumatatu.