Kwa muda wa majuma kadhaa, wakaazi wa mji wa kitalii wa Mtwapa wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kushambuliwa na baadhi ya wahalifu wanaodaiwa kujihami kwa silaha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mmoja kati ya wahalifu hao ni mwanamume aliyetajwa kuwa hatari zaidi kwani kulingana na wakaazi, amekuwa akibeba silaha kama vile panga na shoka huku akiwavamia wapita njia.

Siku ya Jumatano, maafisa wa polisi kutoka Kituo cha polisi cha Mtwapa walifanikiwa kumkamata jamaa huyo aliyetambuliwa kama Peter Babiri.

Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, afisa wa upelelezi kituoni humo Jason Mworya, alisema wanaendelea kumzuilia Babiri, ambaye jina lake la utani ni ‘Kam Kuja’, huku wakiendelea na uchunguzi kabla kumfungulia mashtaka.

Mworya alitoa wito kwa wananchi wanaodai kuvamiwa na mshukiwa huyo kuandikisha ripoti katika vituo vya polisi.

“Ni kweli tumekuwa tukipokea taarifa za uvamizi kutoka kwa wananchi dhidi ya kijana huyu, lakini kwa sasa tunasubiri watu wajitokeze na kudhibitisha madai hayo, ili tuwe na ushahidi wa kumfikisha mahakamani,” alisema Mworya.

Kwa upande wake, Raphael Gona, mzee wa mika 62 kutoka kijiji cha Kandara, alidai kuwa aliwahi kuvamiwa na na mshukiwa huyo.

“Alinivamia usiku lakini kulikuwa na taa inawaka kwa hivyo nilimuona vizuri. Hata nilipoenda pale kituoni, niliweza kumtambua,” alisema mzee Gona.

Afisa huyo wa upelelezi amesema kuwa maafisa wake wamefika mahakamani kuomba muda wa kumzuilia mshukiwa huyo zaidi ili waweze kukamilisha uchunguzi wao.