Mshukiwa wa kundi la kigaidi la al-Shabaab ameuawa baada ya kujaribu kuvamia kituo cha polisi cha Kombani, eneo bunge la Matuga.
Maafisa wa polisi watatu pia wameripotiwa kujeruhiwa kwenye makabilano hayo.
Kijana huyo anadaiwa kuwa miongoni mwa wahalifu waliokua wamejihami kwa panga na mikuki, kwa nia ya kuvamia kituo hicho, usiku wa kuamkia Ijumaa.
Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa Kaunti ya Kwale Kutswa Olaka alisema kuwa wahalifu hao walisikika wakiimba nyimbo zenye asili za kiarabu.
Olaka amelitaja genge hilo kama hatari na ambalo limepokea mafunzo ya ugaidi nchini Somalia.
“Ni genge hatari ambalo limepata mafunzo ya kivita nchini Somalia,” alisema Olaka.
Hata hivyo, alisema juhudi za genge hilo kuvamia kituo hicho zilizimwa pale maafisa waliokuwa wakishika doria waliwakabili na kufanikiwa kumuua mmoja wa washukiwa.
“Genge hilo lilikabiliwa vikali na maafisa wa usalama na mmoja wao kuuawa, huku polisi watatu wakipata majeraha,” alisema Olaka.
Olaka alisema kuwa uchunguzi umeanza kuwasaka wahalifu hao, na kuongeza kuwa watafanya kikao na wakaazi wa Kombani kujadili swala hilo.