Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshukiwa wa mauwaji ya Mpeketoni alielezea mahakama kuwa alinusurika kifo kutoka kwa al-Shabaab baada ya kusoma Quran.

Akitoa ushahidi wake siku ya Jumatatu katika Mahakama kuu ya Mombasa, mshtakiwa, Diana Salim, aliambia mahakama kuwa walivamiwa na wanamgambo akiwa na wenzake katika eneo la Mambosa na kulazimishwa kusoma suratul Fathia.

Salim alisema kuwa wenzake wawili walipigwa risasi baada ya kutambulika kuwa si waislamu.

Alisisitiza kuwa gari zao mbili aina ya matatu zilichukuliwa na wanamgambo hao baada ya kuwavamia.

Aidha, aliwalaumu maafisa wa usalama kwa kumkamata na kumuhusisha na mauwaji hayo, licha ya yeye kuwa nusura na kupiga ripoti katika Kituo cha polisi cha Lamu.

Mahadi Swaleh, mshtakiwa, kwa upande wake alisisitiza kutohusika na mauwaji hayo na kuitaja hatua hiyo kama njama ya kumchafulia jina ikizingatiwa yeye ni mfanyibiashara maarufu katika Kaunti ya Lamu.

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita, mahakama kuu iliwapata na kesi ya kujibu washukiwa hao kuhusiana na mauwaji ya Mpeketoni baada ya mashahidi 32 kukamilisha ushahidi wa kesi hiyo.

Mahadi Swaleh na Diana Salim wanakabiliwa na kesi ya ugaidi na mauwaji ya watu 60 kwenye shambulizi liliotokea Mpeketoni mwaka 2014.