Mahakama ya Mombasa imemuachilia huru mshukiwa wa ubakaji wa mtoto wa miaka 12 baada ya ushahidi kutofautiana.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Jackson Makau anadaiwa kutekeleza ubakaji huo kati ya Oktoba 15 na 17 mwaka wa 2012, katika eneo la Hamisi Estate huko Changamwe.

Aidha, anakabiliwa na shtaka la pili la kumteka nyara mtoto huyo mnamo Oktoba 15 mwaka 2012, na kumfungia chumbani mwake kwa siku tatu.

Hakimu Henry Nyakweba alisema kuwa ushahidi uliotolewa haulingani na ni wazi kuwa mshukiwa huyo hakuhusika katika visa hivyo.

“Mashahidi wa kesi hii walitofautiana pakubwa katika ushahidi wao na kuiweka kesi hii kwenye njia panda,” alisema Hakimu Nyakweba.

“Hatujui nani mkweli kati ya daktari na mtoto, ikizingatiwa mtoto anasema alibakwa sehemu ya mbele, huku uchunguzi wa daktari unaonyesha aliingiliwa katika sehemu yake ya nyuma,” alisema Nyakweba.

Aidha, alisema kuwa itakuwa vigumu kukubali kuwa mtoto huyo alizuiliwa chumbani humo kwa siku tatu bila kutafuta usaidizi kutoka kwa majirani.

“Kwanini mtoto huyo alifungiwa chumbani kwa siku tatu pasi ya kupiga kamsa au kutafuta usaidizi,” alisema Nyakweba.