Mwanamume mmoja alifikishwa katika mahakama ya mjini Mombasa kwa madai ya kumnajisi mtoto wa umri wa miaka minne na nusu.
Inadaiwa kuwa mnamo tarehe Oktoba 4, 2015 katika eneo la Likoni Kaunti ya Mombasa, mshukiwa Richard Musilu alitekeleza kitendo hicho na kutoweka kabla ya kutiwa nguvuni na maafisa wa polisi.
Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Susan Shitubi siku ya Alhamisi, mshukiwa aliyakana madai hayo na kuiomba mahakama imuachilie kwa dhamana.
“Madai yaliyotajwa mbele ya mahakama kuhusu kumnajisi mtoto wa umri wa miaka minnee ni madai ya uongo kwa sababu sijawahi tenda kosa kama hilo. Kutokana na sababu zangu za kiafya, ningeomba mahakama iniwachile kwa dhamana,” alisema Musilu.
Hakimu Shitubi alikubali ombi hilo na kumwachilia kwa dhamana ya Sh300,000 pamoja na mdhamini wa kiasi sawia na hicho ama mshukiwa aendelea kusikiza kesi hiyo akiwa gerezani.
Aidha, alidokeza kuwa anasubiri kukamilika kwa uchunguzi wa maafisa wa upelelezi pamoja na ripoti kamali kutoka kwa madaktari kabla ya kusikiza kesi hiyo vyema na kutoa uamuzi mwafaka.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe Oktoba 29 na kusikizwa Novemba 3, 2015.