Mwanamume anayekabiliwa na madai ya ubakaji wa msichana anayeugua ugonjwa wa kifafa, amepewa muda wa wiki moja kupendekeza kifungo chake.
Juma Ali Juma, ambaye ni mjomba wa msichana huyo, anadaiwa kutekeleza kosa hilo mnamo Februari 6, mwaka huu katika eneo la Mtongwe.
Hii ni baada ya mwendesha mashtaka kutoka afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Erick Masila, kumkabidhi nakala ya mapendekezo ya jinsi mshtakiwa huyo anafaa kuhukumiwa.
Siku ya Alhamisi, mwendesha mashtaka Masila alipendekeza mshukiwa huyo kuhukumiwa maisha kwa kosa hilo linalomkabili.
Juma, ameiomba mahakama kumpa muda wa wiki moja ili kujibu ombi hilo la mwendesha mashtaka.
Hakimu mkuu katika mahakama ya Mombasa Teresia Matheka amekubali ombi hilo na kuagiza kesi hiyo kutajwa siku ya Alhamisi juma lijalo.
Juma lililopita, mahakama hiyo ilimpata mshukiwa huyo na hatia ya ubakaji.