Jengo la Mahakama ya Mombasa. Hakimu Makori alisema kuwa aliafikia uamuzi huo kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kutosha. [Picha/ kenyans.co.ke]
Mshukiwa wa ugaidi anayedaiwa kunaswa na simu yenye video za mafunzo ya kigaidi ameachiliwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha.Rollins Alikula Lubembe anadaiwa kupatikana na video zenye mafunzo ya kigaidi ya kundi la al-Shabaab mnamo Juni 3, 2015 katika eneo la Tudor.Lubembe amekaa rumande kwa takriban miaka miwili tangu kukamatwa kwake mwaka 2015.Akitoa uamuzi wake siku ya Alhamisi, Hakimu mkuu katika Mahakama ya Mombasa Evance Makori alisema kuwa aliafikia uamuzi huo baada ya mashahidi wanane wa kesi hiyo kutofautiana kwenye ushahidi wao.“Mashahidi wote wanane waliotoa ushahidi wao kwenye kesi hii walitofautiana hasa kuhusu aiana ya simu inayodaiwa kunaswa na mshukiwa wa kesi hii,” alisema Makori.Aidha, hakimu huyo alisema kuwa afisi ya mwendesha mashtaka pamoja na afisi za uchunguzi zilikosa kuweka wazi iwapo kungelitokea kisa cha ugaidi ambacho kingesababishwa na mshukiwa huyo.Aidha, Hakimu Makori alisema kuwa hakuna ushahidi unaonyesha kuwa video hizo zinazodaiwa kuwa za ugaidi zilisambazwa kutoka kwa kundi lolote la ugaidi.Vile vile maafisa hao walishindwa kudhibitisha iwapo simu hiyo ilikua ya Lubembe.