Kesi ya ugaidi inayowakabili wasichana wanne waliotiwa mbaroni katika mpaka wa Kenya na Somalia imekosa kuendelea baada ya mmoja wao kuugua.
Hii ni baada ya Mariam Said Aboud, kuondolewa mahakamani kutokana na ugonjwa anaougua kwa sasa.
Mwendesha mashtaka Ngina Mtua ameiambia mahakama kuwa kesi hiyo inafaa kuahirishwa hadi mshukiwa huyo atakapopata nafuu.
“Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma haiwezi kuendelea na kesi hiyo hadi pale Bi Aboud atakapofika mbele ya mahakama hii,” alisema Ngina.
Wakili wa washukiwa hao, Hamisi Mwadzogo, alipinga ombi hilo na kusisitiza kesi hiyo kuendelea kama ilivyopangwa.
“Hii kesi ni ya kitambo na yapaswa kuendelea licha ya mmoja wa washukiwa kutohudhuria kikao hiki,” alisema Mwadzogo.
Hakimu Daglous Ogoti hatahivyo aliagiza kesi hiyo kuahirishwa hadi mnamo Oktoba 10, 2017, itakapotajwa.
Washukiwa hao wamesalia rumande tangu mwaka jana, walipotiwa mbaroni.
Wanne hao, Ummulkheir Abdullah kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 21, Mariam Said Aboud pamoja na Khadija Abubakar wenye umri wa miaka 19 wote kutoka Malindi wanadaiwa kuwa wanafunzi walioahidiwa ufadhili wa kimasomo nchini Somalia, huku Halima Aden akikamatwa katika kaunti ya Machakos kwa tuhuma za ugaidi.