Kesi dhidi ya mshukiwa wa kusambaza vitisho vya kigaidi katika chuo kikuu cha Egerton, haikuendelea Jumatatu baada ya wakili wa upande wa utetezi kukosa kufika mahakamani.
Wakili David Mongeri alikuwa ametaka kutengewa tarehe katika kikao cha awali mahakamani, kuwasilisha stakabadhi zake kwa mara ya mwisho kabla ya kesi hiyo kufungwa.
Mashahidi wote katika kesi hiyo wametoa ushahidi wao.
Inspekta Joseph Kolum kutoka kitengo cha upelelezi cha CID ndiye alikuwa wa mwisho kutoa ushahidi wake mnamo tarehe 26 Januari,2016.
Inspekta Kolum aliambia mahakama kwamba habari alizopata kwenye ukurasa wa Facebook wa mshtakiwa Robert Mungai maarufu kama Mohammed Bluez, zilikuwa zenye uzito mkubwa ikizingatiwa vitendo vya kigaidi.
Kolum pia alieleza mahakama kwamba mshukiwa alikuwa amezungumzia jinsi magaidi wa Al-Shabaab wangevamia chuo kikuu cha Egerton huko Njoro na kwamba shambulizi hilo lingekuwa kubwa kuliko lile la chuo kikuu cha Moi bewa la Garrisa.
Robert Mungai anakabiliwa na mashtaka ya kueneza jumbe hizo za kigaidi kwenye akaunti yake ya Facebook.
Kesi hiyo itasikilizwa tena mnamo Machi,1,2016.