Polisi mjini Nyamira wamemtia mbaroni mwanamke mmoja aliyeshukiwa kuwalaghai wakazi kwa kuwahadaa kuwatafutia kazi kwenye hospitali ya mkoa, kule Nakuru.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, OCPD wa Nyamira Bw Ricoh Ngare alisema kuwa mwanamke huyo ambaye anadaiwa alikuwa anajifanya kuwa afisa wa masuala ya kliniki alikuwa amewahadaa wanakanisa wa kanisa la Kiadventista la Rirumi kule Kebirigo, kwa kuwaambia kuwa hospitali hiyo ilikuwa na nafasi za kazi za manesi makatibu na wahudumu wa maabara.
"Mshukiwa ambaye tumemtia mbaroni alikuwa tayari amewahadaa pesa wanakanisa wa kanisa la Kiadventista la Rirumi kule kebirigo kwa kuwadanganya kuwa hospitali kuu ya Nakuru ilikuwa na nafasi za kazi,” alisema Ngare.
Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa amewadanganya watu kuwa nafasi hizo zingepeanwa kwa malipo ya Sh7,500 zakugharamia sare za kazi na Sh10,000 za malazi huku akiwahaidi kulipwa Sh28,700 kila mwezi.
"Mshukiwa alikuwa amewahadaa wananchi kati ya Sh175,000 kwa kuwa alikuwa akiitisha kati ya Sh10,000 na Sh45,000,” alisema Ngare.
Ngare alisema kuwa baada ya mahojiano ya muda mrefu maafisa wa upelelezi waligundua kuwa mshukiwa huyo wa ulaghai alikuwa na cheti cha matibabu na pia stashahada ya upasuaji wanazozishuku kuwa sio halali.
"Maafisa wa upelelezi waligundua kuwa mshukiwa alikuwa na cheti cha matibabu na stashahada ya upasuaji ila wanashuku kuwa vyeti hivyo sio halali. Tunaendelea na uchunguzi na tutamfikisha mahakamani siku ya Ijumaa,” alisema Ngare.