Jengo la mahakama ya Mombasa.[Picha/the-star.co.ke]
Mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya amehukumiwa kifungo cha miaka nane gerezani.
Isiah Obala Oluoch anadaiwa mnamo Septemba 20, 2014,alipatikana na misokoto 16 ya bangi yenye thamani ya shilingi 32,000 katika eneo la Magongo eneo bunge la Changamwe.
Akitoa hukumu hiyo siku ya Jumatatu,hakimu Edgar Kagoni katika mahakama ya Mombasa, alisema kuwa kulingana na ushahidi uliotolewa ni wazi kuwa mshukiwa alipatikana na bangi hiyo.
“Ushahhidi uliotolewa ni wazi mshukiwa alihusika katika ulanguzi wa bangi hiyo”,alisema Kagoni.
Aidha,ameitaja hukumu hiyo kuwa funzo kwa wengine wenye biashara ya ulanguzi wa mihadharati eneo la Mombasa.
“Kifungo hiki kitakuwa funzo kwa wale wanaoendeleza biashara za mihadharatikatika kaunti hii”,alisema Kagoni.
Aliongeza kuwa vijana wengi eneo la Mombasa wameharibika kutokana na utumizi wa mihadharati.
“Vijana wengi wamepotea kwa utumizi wa mihadharati,wengi wameacha masomo kwa sababu ya kuvuta bangi”,alisema Kagoni.
Alisema kuwa idara ya mahakama itahakiisha walanguzi wa dawa za kulevya hawatasazwa punde wakifikishwa mahakamani.