Mwanamume mmoja katika eneo la Athena kaunti ya Kiambu ametiwa mbaroni asubuhi ya kuamkia jana baada ya kuteka nyara na kumnajisi msichana wa miaka 14 kwa muda wa siku tano.
Mwanamume huyo, Jonah Mwangi, alifumaniwa nyumbani kwake na maafisa wa polisi huku wameandamana na mamake msichana huyo. Mshukiwa huyo baada ya kuwaona maafisa wa polisi alijaribu kutorokea mlango wa nyuma lakini akapata umati wa watu umejaa nje ukimngoja.
Duru za kuaminika zinaarifu kuwa hii sio mara ya kwanza kwa mwanamume huyo kupatikana na kosa la aina hii kwani mwaka uliopita alitiwa mbaroni baada ya kumfungia msichana wa miaka kumi na mitano lakini baadaye kuachiliwa kwa sababu zisizojulikana.
"Alhamisi mwanangu alinijulisha kuwa alitaka kumtembelea rafikiye ili akafanye kazi ya ziada waliokuwa wamepewa shuleni lakini hakurejea nyumbani," Alisema mamake msichana huyo.
Aliongezea, "Baada ya kumkosa mwanangu shuleni, niliulizia marafiki zake na ndipo wakanielekeza nyumbani kwa mtu huyo pale nilichukua hatua ya kuja na maafisa wa polisi ili atiwe mbaroni."
Wakaazi wa eneo hili wanadai kuwa kucheleweshwa kwa kufunguliwa kwa kituo cha polisi ambacho kishamalizika kujengwa ndiko kunachangia visa kama hivi kutokea.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Thika akisubiri kufikishwa mahakamani.