Mlinzi mmoja ameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kuiba mali ya mwajiri wake.
Upande wa mashtaka ulielezea mahakama siku ya Jumatatu kuwa mshtakiwa, Maina Njeru, anadaiwa kuiba mali ya mwajiri wake Nasifa Mohamed, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne tarehe 7 mwezi Mei, katika eneo la Kizingo jijini Mombasa.
Aidha, mshukiwa huyo alikabiliwa na shtaka mbadala la kukosa kuzuia uhalifu.
Bwana Njeru alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Douglas Ogoti.
Hakimu Ogoti aliagiza mshukiwa huyo kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja au shilingi laki tano pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 19 mwezi Mei.