Wakaazi waliojawa na ghadhabu katika eneo la Majengo mapya huko Likoni, wamemshambulia na kumuua mwanamume mmoja aliyehusishwa na wizi.
Kulingana na walioshuhudia kisa kicho, mshukiwa huyo anadaiwa kujaribu kumuibia msichana mmoja huku akiwa amejihami kwa kisu.
Inaripotiwa kuwa msichana huyo alikuwa akisafirisha bidhaa zake za nyumba kuhamia sehemu nyingine kabla ya marehemu kujaribu kumuibia.
Akithibitisha kisa hicho, Afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni, Willy Simba, alisema kuwa tayari maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.
"Tumeanzisha uchunguzi kuhusiana na kisha hicho lakini tunawaamba wakaazi kuripoti kwa maafisa wetu wanapomkamata mshukiwa wa wizi,” alisema Simba siku ya Jumatatu.
Aidha, amewataka wakaazi kukoma kuchukua hatua mikononi mwao wanapojawa na hasira na kuwafikisha wahalifu kwa maafisa wa polisi ili kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali kuu ya Pwani mjini Mombasa.