Mwanamme mmoja mwenye umri wa makamo ambaye ni mshukiwa wa wizi anaendelea kupigania maisha yake kwenye hospitali kuu ya Nyamira kufuatia majeraha mabaya ya moto aliyoyapata baada ya wananchi waliokuwa na hamaki kumshambulia.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yalijiri baada ya mwanamme huyo alifumaniwa akijaribu kuiba ndani ya boma la mfanyibiashara mmoja katika sehemu ya Tente, mjini Nyamira. 

Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatano OCPD wa Nyamira Rico Ngare alisema kuwa mshukiwa huyo aliyekuwa ameandamana na wenzake waliofanikiwa kutoroka, walifika kwa boma la mfanyibiashara maarufu Julius Mokaya saa mbili unusu usiku kwa kuruka juu ya lango kuu, lakini kwa bahati nzuri mlinzi akawaona na kupiga kamsa ambapo wananchi walifika kwa haraka na kumteketeza.

"Mshukiwa wa wizi ambaye angali anapigania maisha yake kwenye hospitali kuu ya Nyamira alikabiliwa na wananchi wenye ghadhabu baada ya washukiwa wenzake waliokuwa na njama ya kuiba kutoka kwa boma ya mfanyabiashara Mokaya kutoweka," alisema Ngare. 

Ngare aidha alisema maafisa wa polisi walifika kwa haraka na kumwokoa kabla hajateketea sana huku wenzake wakitoroka kwa kutumia pikipiki na uchunguzi umeanzishwa.

"Uzuru ni kwamba maafisa wa polisi walifika katika eneo la tukio kwa haraka na kumuokoa mshukiwa na tayari uchunguzi umeanzishwa ili kuwatia mbaroni washukiwa wengine waliotoweka," aliongezea Ngare.