Share news tips with us here at Hivisasa

Msichana mmoja amefikishwa mahakamani kujibu shtaka la kujaribu kumuua jirani yake.

Mshtakiwa huyo mwenye umri wa miaka 17, anadaiwa kujaribu kumuua jirani yake mwenye umri wa miaka 69, kwa kumtishia mnamo Julai, 2015.

Upande wa mashtaka ulielezea mahakama siku ya Jumanne kwamba mshtakiwa, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne, anadaiwa kumtishia jirani yake, Margaret Wanjiru, kuwa angemkata kichwa iwapo hangempa shillingi elfu tisini, mnamo Julai 7, 2015 katika eneo la Mang’u, Kaunti ya Nakuru.

Msichana huyo hata hivyo alikana shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkuu Doreen Mulekyo wa mahakama ya Nakuru.

Hakimu Mulekyo aliagiza msichana huyo awekwe chini ya ulinzi wa wazazi wake kutokana na umri wake.

Aidha, aliagiza kesi hiyo itajwe tarehe Desemba 1, 2015 na kusema kwamba siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo itatolewa siku hiyo.