Msichana mwenye umri wa miaka 13 kutoka familia moja maskini kwenye makaazi ya vibanda ya Kiratina mjini Nakuru, huenda akakosa kuendelea na masomo yake ikiwa hatapata ufadhili.
Grace Mbone alijizolea jumla ya alama 421 baada ya kufanya mtihani wa KCPE katika shule ya msingi ya umma ya St John’s, na ndoto yake ni kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Alliance.
Grace alidhihirisha ushindi huo kwa kuwabwaga wenzake 151, na vile vile uongozi kwani kabla ya kufanya mtihani huo alikuwa spika wa baraza la wanafunzi katika kaunti ya Nakuru.
Familia yake sasa inaomba msaada kutoka kwa mashirika ya kijamii, yale yasiyo ya kiserikali ama wahisani wema, ili aweze kujiunga na shule ya upili.
Wito wa familia hiyo umetiliwa mkazo na mwalimu mkuu wa shule hiyo Benta Atieno, akisema mwanafunzi huyo ana uwezo wa kuwa kiongozi bora nchini siku za usoni.
“Wanafunzi wengi katika shule hii hutoka kwenye mitaa duni, na kwa hivyo kuna haja kwa viongozi kusaidia wanafunzi welevu kama yeye” alisema Bi Atieno akiongea na mwandishi huyu Ijumaa.
Rais wa baraza hilo la wanafunzi katika kaunti ya Nakuru John Chate ambaye alipata alama 416 vile vile anapania kutafuta usaidizi kutoka kwa jamii yake ya Kusini mwa Sudan, ili kujiunga na shule ya wavulana ya Starehe. Chate pia anatoka shule iyo hiyo ya st. John's