Mwanafunzi mmoja wa umri wa miaka 17 wa shule ya upili ya Mariindi iliyoko Mugirango Magharibi, Nyamira, amejitoa uhai kwa kujirusha ndani ya choo cha shule hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Inasemekana Judy Maasi alijirusha kwa choo hicho cha futi 60 Jumapili asubuhi.

Akithibithisha kisa hicho, OCPD wa Nyamira, Ricah Ong’are, alisema mwanafunzi huyo aliyekuwa katika kidato cha tatu katika shule hiyo alijiua siku ya Jumapili mwendo wa saa 12:00. Hii ni baada ya kupatikana bwenini akiongea kwa simu usiku wa kuamkia Jumapili, jambo ambalo ni kinyume na sheria za shule hiyo

Inasemekana msichana huyo aliamua kujitoa uhai kwa kuogopa kuchukuliwa hatua kwa kutumia simu shuleni.

“Msichana huyo alipatikana na simu kitendo ambacho ni kinyume na sheria za shule hii. Leo asubuhi akaambiwa alete wazazi wake na huenda ndio ilimtatiza akili na akaamua kujirusha ndani ya choo,” alisema Ong'are.

“Alifungua ile shimo yenye inatumika kutoa uchafu kutoka ndani ya choo (Sceptic tank) ndiposa akajirusha mle ndani na kufariki,” aliongeza Ong'are.

Mwili wa marehemu huyo ulitolewa ndani ya choo hicho na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nyamira, hayo ni kwa mujibu wa OCPD Ngare.