Waziri wa elimu Fred Matiang'i.[Photo/Nation]

Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa yaani day schools wametakiwa kutolipa hata shilingi moja kwa shule hizo kwani serikali imeshawalipia karo wanafunzi hao.

Kauli hii imetolewa na kaimu waziri wa elimu Dktr Fred Matiang’i alipokutana na washikadau wa elimu pamoja na viongozi wa eneo la Pwani katika shule ya kiserikali jijini Mombasa siku ya Jumatano.

Matiang’i amedokeza kuwa tayari wizara ya elimu imewaagiza maafisa wa elimu kuanzisha msako dhidi ya shule za kutwa zinazowatoza wanafunzi pesa zozote.

Amesisistiza kuwa serikali imemlipia kila mwanafunzi anayejiunga na kidato cha kwanza shilingi 22 240, hivyo basi hakuna haja ya mwanafunzi kutozwa pesa tena shuleni.

Alisema hatua ya serikali kumlipia kila mwanafunz shilingi 22,240 ni ya kuhakikisha wanafunzi wote waliomaliza darasa la 8 wanajiunga na kidato cha kwanza kwa asilimia 100 bila malipo yoyote.

Matiang’i ameonya shule zinazowatoza wanafunzi hao pesa zozote kuwa zinafanya makosa na kwamba huenda zikachukuliwa hatua za kisheria.