Kizaazaa kilishuhudiwa mapema Jumatatu kwenye afisi ya gavana wa kaunti ya Nyamira baada ya msimamizi wa wafanyikazi kwenye kaunti hiyo Kennedy Ongaga kujificha afisini mwa gavana ili kukwepa kutiwa mbaroni.
Akihutubia wanahabari afisini mwake, kamanda mshirikishi wa maafisa wa polisi wa utawala kwenye kaunti hiyo Kalimbo Mwandoye alisema kuwa ni kweli afisa huyo alitiwa mbaroni na anatarajiwa kufikishwa mahakami hii leo, Jumanne, kujibu mashtaka ya tuhuma kwamba aliharibu vitu za nyumbani za nduguye.
"Ni kweli kuwa Ongaga ametiwa mbaroni na maafisa wangu wa polisi baada yake kujifungia afisini mwa gavana Nyagarama kwa saa tatu ili kukwepa kutiwa mbaroni na maafisa wa polisi, na hili ni kutokana na hatua yake ya kupasua runinga, vyombo vya nyumbani na radio aina ya 'home theatre'," alisema Mwandoye.
Mwandoye aliongeza kusema kuwa afisa huyo sharti afikishwe mahakamani kujibu mashtaka yatakayomkabili kwa kuwa hamna mtu yeyote ambaye ni mkubwa kuliko sheria za kenya.
Shughuli za kawaida zilisitishwa kwa muda afisini mwa gavana Nyagarama baada ya afisa huyo kukataa kujiwasilisha kwa polisi, hali iliyomlazimu mkuu wa polisi wa kituo cha cha Nyamira Alex Mumo kuingilia kati na kumtia nguvuni afisa huyo na kisha kumuwasilisha kwenye kituo cha polisi cha Nyamira kuandikisha ripoti.
Haya yanajiri baada ya afisa huyo kukwepa mitego kadhaa ya polisi kumtia mbaroni, baada ya ilani ya kumtia mbaroni kutolewa wiki moja iliyopita.