Jamii ya Kisii imeshauriwa kutowapigia kura wanasiasa ambao wanawadanganya wakenya kuandamana ili kujifaidi kisiasa.
Ushauri huo umetolewa baada ya viongozi wa mrengo wa Cord kuandaa maandamano juma lililopita mjini Nairobi kushinikiza makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) kuondoka afisini.
Kulingana na Waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i aliyezungumza mjini Nyamira aliomba jamii ya Gusii kutowapigia kura aina ya wanasiasa wanaowadanganya wakenya kuandamana bila kufuata utaratibu.
“Haiwezekana baadhi ya wanasiasa kudanganya wakenya kuacha biashara, kusomesha watoto, kufanya kilimo na kuanza kuandamana barabarani kama watu wasio na la kufanya hatutakubali hayo,” alisema Matiang’i.
“Naomba jamii yetu ya Gusii kutodanganywa kuandamana tuna kazi za kufanya ambazo zinatufaidi na msiwapigie kura wanasiasa wanaoandamana bila sababu halisi wale wa kuandamana hawana kazi ya kufanya naomba muachane nao,” aliongeza Matiang’i.
Aidha, Matiang’i alikosoa muungano wa Cord kwa kuhitaji kugawana wakenya kwa msingi isiyofaa na kuomba wakenya kusimama na kuchagua busara.