Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku zoezi la kuwapa chanjo ya polio watoto walio chini ya umri wa miaka mitano likiendelea kupata upinzani kutoka kwa jumuia ya dini nchini, wakazi wa Kaunti ya Nyamira wameombwa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo.

Chanjo hiyo itafanyika siku ya Jumamosi tarehe moja mwezi Agosti.

Akiongea siku ya Jumatano jioni katika ofisi yake mjini Nyamira, mkurugenzi mkuu wa afya katika katika kaunti hiyo Jack Magara aliwataka wazazi na walezi walio na watoto wenye umri huo kupuuza wito wa viongozi wa makanisa na kuhudhuria hafla hiyo ili kuwasaidia wanao kuepuka na maradhi ya kupooza. 

"Ningependa kuwaomba wazazi wote kuhakikisha watoto wao wanaletwa katika vituo husika vya afya ili kupata chanjo dhidi ya maradhi ya polio. Msipotoshwe na watu wa makanisa ambao wanaendelea kupinga zoezi hili," alihoji Magara.

Mkurugenzi huyo alieleza umuhimu wa wazazi kupewa ujumbe ufaao kuhusiana na zoezi hilo kutoka kwa wajuzi na wataalam wa masuala ya afya akisema wengi wa wazazi na walezi wachagua kuwafuata viongozi wa makanisa badala ya kuwasikiliza wataalam wa afya.

Hata hivyo, Bw Magara alionyesha matumaini yake kuwa hata kama baadhi ya wahusika wamechochewa, juhudi za wizara ya afya kwa ushirikiano na idara tofauti za Kaunti ya Nyamira zitazalisha matunda mema hatimaye na kuwasihi walio na nia njema kuwashauri wazazi kuwapeleka wao kupata chanjo.