Share news tips with us here at Hivisasa

Mamia ya wasafiri waliokwama kwenye msongamano wa magari katika barabara ya Nairobi-Mombasa wameitaka serikali kushughulikia tatizo hilo linalotokea mara kwa mara.

Abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea mjini Mombasa wamelalamikia hali hiyo huku wakisema kuwa biashara zao ziliathirika kutokana na hali hiyo.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu, abiria hao walisema kuwa walikesha barabarani usiku kucha bila hatua yoyote kuchukuliwa.

“Tulikuwa tunasafiri kutoka Nairobi kuja Mombasa. Msongamano ulianza saa tatu usiku na hakuna lolote limefanyika. Kwa sasa shughuli zetu zimetatizika kabisa,” alisema Alfred Otieno, mmoja wa wasafiri.

Msongamano huo unadaiwa kuanzia eneo la Athi River hadi sehemu ya Maanzoni, jambo ambalo abiria hao walisema lilisababishwa na ajali iliyohusisha lori tatu eneo hilo.

Shughuli katika kituo cha mabasi cha Mwembe Tayari mjini Mombasa pia zilitatizika kwa saa kadhaa baada ya basi za kutoka Nairobi na maeneo mengine kuchelewa kufika katika saa zilizotarajiwa kuwasili.

Barabara ya Mombasa-Nairobi hutegemewa zaidi katika usafiri wa abiria na mizigo kutoka na kuingia mjini Mombasa.

Barabara hiyo hutumiwa kuunganiisha mji wa Mombasa na miji mingine mikuu nchini na kila kunapotokea msongamano, shughuli nyingi za kibiashara hutatizika pakubwa.