Katibu mratibu wa chama cha mashamba makubwa makubwa nchini Henry Omasire amejitokeza kuwarahi wafanyakazi wa mashamba ya chai kuzingatia utulivu ili kungoja kulipwa mishahara yao.
Hii ni kufuatia kuwepo kwa kesi kati ya chama hicho na kampuni ya Chai ya Uniliver pamoja na shirikisho la wamiliki wa zao la chai nchini KTGA kwenye mahakama ya viwanda nchini kuhusu nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi.
Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumanne, Omasire aliwahimiza wafanyakazi hasa katika eneo la Sotik, Kericho, Nandi hills na Limuru kuwa watulivu chama hicho kinapoendelea kupambana na waajiri mahakamani.
"Kuna kesi kati yetu na kampuni ya Uniliver pamoja na shirikisho la wamiliki wa chai KTGA ambayo imekuwa mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili ila nina imani kwamba kesi hiyo itakamilika hivi karibuni, na ni ombi langu kwa wafanyakazi kuzingatia utulivu hadi kesi hiyo itakapo tamatika," alisema Omasire.
Omasire aidha aliongeza kwa kurahi kampuni za chai nchini kuajiri wafanyakazi zaidi hasa kwenye msimu huu wa mvua.
"Sote tunafahamu kuwa huu ni msimu wa mvua na zao la chai linazidi kuongezeka na ndio maana narahi kampuni za umiliki wa chai kuajiri wafanyakazi wengi ili kuchuna chai kama njia mojawapo yakubuni nafasi za ajira," aliongezea Omasire.