Kila anayetegea anga za 90.7 Mombasa bila shaka anaifahamu sauti ya sura hii.
Sammy Mwaura, mtangazaji katika idhaa ya Radio Salaam 90.7 Mombasa, anayekuletea taarifa za habari kila siku ya wiki katika kipindi Leo Radio Salaam, ameendelea kuuchukua umati wa wapenzi wa kituo hicho kwa ufasaha alionao katika tasnia ya uandishi wa habari.
Amekuwa kwenye tanzu ya kufahamisha wananchi yanayojiri kwa muda wa miaka mitano sasa.
Alisema kuwa yeye hufurahishwa zaidi pale anapojadiliana na mtu asiyemuona.
Ushawai jiuliza yepi aliyopitia hadi kufikia mahali alipo sasa?
Mwaura anakiri kuwa hakuna kitu rahisi maishani bila ya kujituma kwa kila jambo.
Anaitaja fani ya utangazaji kama inayohitaji kujiamini na zaidi ya yoyote inayohitaji kwa kiasi kikubwa ukakamavu.
“Kila kukicha namna vituo vya radio vinavyofunguliwa ndivyo wanahabari wanavyofuzu kutoka vyuo mbalimbali,” alisema Mwaura.
Aidha, ametaja kazi ya utangazaji kama yenye ushindani mkali, kwani mara nyingi huwa waajiri wanazingatia kipaji wala sio elimu kama ilivyo desturi katika kazi nyengine.
Mwaura aliwashauri wale wanaopania kuwa watangazaji kwa kusema kuwa mtangazaji bora lazima kwanza aipende kazi hiyo na kuonesha tofauti katika fani hiyo.