Mvua nyingi iliyonyesha siku ya Alhamisi jioni nusura isababishe maafa baada ya Mto Nyakumisaro kuvunja kingo zake na kufunga daraja linalounganisha barabara ya Ram na lile ya kuelekea Magereza ambapo iliwabidi wanaolitumia barabara hilo kuvushwa na Bodaboda.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mafuriko hayo yalishuhudia msongamano wa magari na mlolongo wa watu waliosubiri Bodaboda kuwavusha upande wa pili wa barabara kwani wanaoendesha Bodaboda walivuna pesa nyingi kufuatia hali hiyo.

Hata hivyo kulishuhudiwa kioja pale muendesha Bodaboda mmoja aliponea chupu chupu aliposombwa pamoja na Bodaboda yake na maji mengi ambayo yalikuwa yameelea alipokaidi ushauri kutoka kwa wenzake kuwa apitie sehemu ya kushoto ambayo haikuwa na maji mengi. Jamaa huyo kwa bahati nzuri aliokolewa kabla ya kuporomoshwa kwenye mto huo.

Mmoja wa kina mama wanaofanya biashara na kumiliki vibanda kando ya hilo daraja Faith Gesare alisema kuwa hii ni mara ya pili anashuhudia mto huo kujaa kiasi hicho na kuonya wanaotumia barabara hilo hasa wenye Bodaboda kuwa makini wanapovuka daraja hilo wakati wa mvua nyingi.

Jamlek Ombati ambaye ni muendesha Bodaboda kwa upande wake hakufurahishwa na jinsi wenzake walivyoonyesha tamaa ya kutaka kuvusha watu bila kuzingatia usalama na maisha ya abiria wao huku akifananisha tokeo hilo na la Narok ambapo baadhi walipuuza mawaidha ya wengine na kuangamia.

"Hata kama nikutengeneza pesa si vizuri kuweka maisha ya wengine kwenye hatari. Kama sio mimi huyo kijana alikuwa aangamie," alisema Ombati na kuwataka wenzao kumakinika na kujali maisha yao na ya abiria wao.

Dereva wa SmartLine Benson Onsongo ambaye hutumia njia hiyo aliitaka Serikali ya Kaunti ya Kisii kuinua daraja hilo ambalo alidai kuwa limefurika mara nyingi na huenda hivi karibuni lilete maafa makubwa iwapo Serikali ya Kaunti hiyo haitachukua hatua ya mapema kulirekebisha.

"Hii ni mara kama ya tatu nimeshuhudia tukiangaika wakati mto huu unajaa. Mwaka jana tuliahidiwa na Wizara ya barabara kuwa watashughulikia daraja hili lakini bado mambo ni yale yale," alisema Onsongo na kuwatahadharisha wanaoendesha Bodaboda dhidi ya kupuuza ushauri na waweke tamaa ya pesa nyuma.