Mtoto wa umri wa miaka 14 katika mtaa wa Kalahari eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa ameripotiwa kufariki baada ya kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Waliyoshuhudia tukio hilo walisema kuwa mtoto huyo alikuwa akivuka kidaraja kidogo cha kupitisha maji taka akiwa na mwenzake kabla ya kusombwa na maji yaliokuwa yakipita kwa kasi.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika mtaa huo wa Kalahari, Janet Nzioka, mamake mdogo wa kijana huyo alisema kuwa kijana huyo alikuwa kisa hicho kilimshtua sana.
Mariam Nyare, mkaazi wa mtaa huo, alisema kuwa licha ya kupeleka lalama zao kwa idara husika kuhusiana na kurekebishwa kwa mitaro ya maji taka katika eneo hilo, hakuna hatua zozote zilizoweza kuchukuliwa kufikia sasa.
"Tunasikitika sisi kwa kumpoteza mtoto huyu mdogo. Tulitoa lalama zetu kwa idara husika katika Kaunti ya Mombasa na wakatuhakikishia kuwa kunajengwa vidaraja vidogo ili kuwawezesha wakaazi kuvuka wakati wa mvua nyingi,” alisema Nyare.
Shirika la Msalaba Mwekundu limetoa tahadhari kwa wakaazi wa maeneo ya mabonde kuhamia maeneo ya juu pamoja na kuwataka wakaazi kuwa waangalifu na watoto wao hasa msimu huu wa mvua.