Mtoto wa umri wa miaka sita kwa kutoka kijiji cha Nyaisa, Lokesheni ya Morake Wilayani Manga katika Kaunti ya Nyamira amefariki baada ya kuanguka ndani ya Mto Moromba siku ya Alhamisi.
Akithibitisha kisa hicho, Chifu wa Lokesheni hiyo ya Morake Nehemia Ogendi alisema kuwa mtoto huyo alikuwa anacheza na watoto wengine wa shule anayosoma ya Msingi ya Nyaisa huku wakicheza karibu na mto huo na kwa bahati mbaya akateleza na kuanguka ndani ndiposa watoto hao walipiga mayowe yaliowavutia wanakijij kuenda kumuokoa mtoto huyo kutoka kwenye maji hayo lakini juhudi zao hazikufua dafu kwani tayari alikuwa amefariki.
“Mtoto huyo alikuwa anasoma Shule ya Msingi ya Nyaisa akiwa darasa la chekechea lakini kwa bahati mbaya amefariki kwenye ajali hiyo ya maji baada ya kuanguka ndani ya Mto huu wa Moromba,” alihoji Chifu Ogendi.
Aidha, Chifu huyo amewaomba wakaazi wa sehemu hiyo kuwa na utulivu huku akiwaomba wale wanatengeneza matofali pia wawe wakirudisha mchanga ndani ya shimo hizo na kuziba shimo hizo maana hata shimo kama hizo husababisha maafa. Hayo ni baada ya kitendo kama hicho kushuhudiwa katika sehemu hiyo kwa takribani miezi miwili ilyopita.
“Naomba wazazi wawe wakiwafundisha watoto jinsi na sehemu ya kuchezea maana hao hufanya mzaha na wanakufa bila kupanga,” alisema Chifu Ogendi.
Wakaazi wa eneo hilo walijawa na hasira baada ya mtoto huyo kuaga dunia na kutaka dimbwi na shimo kama hizo zizibwe au zingirwe na ua mara moja haswa katika msimu huu wa mvua.