Mbiwi la simanzi lilitanda katika kijiji cha Kiambiriria wilayani Molo, baada ya mtoto mwenye umri wa miaka 15 kujitoa uhai kwa kuruka ndani ya kisima cha maji.
Kwa mjibu wa walioshuhudia kisa hicho, mtoto huyo ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu amekuwa akionekana kuchanganyikiwa kimawazo.
Wakazi wa eneo hilo wamesema mtoto huyo ambaye alitamatisha masomo yake akiwa darasa la sita amekuwa akiishi na nyanyake mwenye umri wa miaka 75, baada ya mamake kufariki miaka tisa iliyopita.
Beatrice Wairimu, pamoja na Irene Wanjiku, ambao ni baadhi ya majirani wanaosaidia ajuza huyo wamesema mtoto huyo amekuwa akiugua, na hivi karibuni amekuwa mwingi wa mawazo huku akitishia kujiua.
Kisa hicho kimethibitishwa na Chifu wa kata ya Kiambiriria Peter Muiruri, ambaye ameuliza wakazi kuwa wangalifu ili kuepuka visa sampuli hiyo.
Maafisa wa polisi, wakiongozwa na afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Molo Stephen Kabii walifika katika eneo la mkasa, na kuanzisha uchunguzi huku mwili huo ukipelekwa katika ufuo wa hospitali ya Molo.