Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyebakwa na babake wa kambo atatoa ushahidi wake wiki ijayo katika Mahakama ya Shanzu.
Mahakama imeagiza mtoto huyo kutoa ushahidi huo siku ya Jumanne juma lijalo, mbele ya Hakimu Diana Mochache.
Siku ya Ijumaa, Mahakama kuu iliagiza mtoto huyo kuwasilishwa katika mahakama kuu ya Mombasa siku ya Jumanne, baada ya kutoa ushahidi wake kabla ya mahakama kusikiliza ombi la kumuachilia kwa dhamana mshukiwa wa ubakaji wa mtoto huyo.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Patrick Otieno alisema kuwa itakuwa vizuri iwapo mtoto huyo atafikishwa mbele yake kabla ya kusikiliza rufaa ya kuachilia kwa dhamana mshukiwa huyo wa ubakaji kwa jina Muhammed Ahmed.
Ahmed anadaiwa kumbaka mtoto huyo katika eneo la Bullo, gatuzi dogo la Kisauni, kati ya mwaka 2013 na Julai mwaka 2015
Mshukiwa huyo wa ubakaji alikata rufaa katika Mahakama Kuu akiomba kuachiliwa kwa dhamana.