Wizara ya elimu katika kaunti ya Mombasa imeahidi kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa wazazi wanaowakandamiza watoto wao wa kike na kuwanyima elimu watakabiliwa kisheria.
Kulingana na waziri wa elimu katika kaunti hiyo Tendai Lewa Mtana, mtoto wa kike ana haki sawa na mtoto wa kiume kupata elimu ili kuhakikisha kuwa ananufaika maishani na kuzisaidia jamii zao.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Tendai amesema kuwa tayari wizara hiyo kupitia serikali ya kaunti ya Mombasa imepanga mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa watoto wa kike hawabaguliwi na swala la taasubi ya kiume inatupiliwa mbali, akisema kuwa mambo hayo yalipitwa na wakati.
Amesema kuwa mila na tamaduni za kale ndizo kwa kiasi kikubwa zinachangia kurudisha nyuma ndoto za watoto wa kike na mara nyingi hujikuta katika ndoa za mapema bila ya kutarajia na akaahidi kuchukua jukumu la kisitisha fikra potovu za jamii mashinani.
“Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tunaahidi kuhakikisha kuwa mtoto wa kike katika kaunti hii inapata elimu sawa na mtoto wa kiume na maswala ya mila na tamaduni za kale tunawaomba wazazi kusahau mambo hayo na kumpa nafasi mtoto wa kike kutimiza ndoto yake maishani,” alisema Tendai.
Tendai hata hivyo ameahidi kutembelea shule zote za msingi na chekechea za umma kuhakikisha kuwa anafanya mazungumza na walimu wakuu hususan kuhusu kuwapa nafasi zaidi watoto wa kike kusoma huku akipanga kuzuru mashinani na kufanya mikutano ya hamasa.