Dereva wa gari moja la kibinafsi aina yaa Mercedes amepoteza maisha yake katika ajali ya barabara iliyotokea Ijumaa mchana katika eneo la Kinari katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.
Watu wengine watatu walijeruhiwa vibaya katika ajali hiyo, ambayo ilihusisha gari mbili, ingine ikiwa gari aina la Prado.
Walioshuhudia ajali hiyo walisema kuwa mwendeshaji wa gari aina la Prado alikuwa anajaribu kupita magari mengine wakati ajali ilitokea, na wakagongana ana kwa ana na hilo la Mercedes.
Majeruhi walipelekwa hospitali ya misheni ya AIC Kijabe kupata matibabu, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika chumba cha maiti cha Naivasha.
Polisi walifika mahali pa tukio na kuelekeza magari kuzuia msongamano wa magari, na pia kuondoa mabaki ya magari hayo barabarani na kuyapeleka katika stesheni ya polisi ya Uplands iliyo karibu na pale.
Mkazi wa Kinari, Kinuthia Waweru alilalamika ongezeko la ajali sehemu hiyo, huku akisema kuwa kuna umuhimu barabara kupanuliwa katika eneo hilo.
“Ni vyema wanaoshughlika na kazi za barabara nchini kupanua barabara hii kwani inatumika na magari mengi ilihali ni ndogo sana,” alisema Waweru.
Naye Benard Onyango alisema ni makosa kwa mtu kufa ilihali kufa kwake kungezuiliwa kwa kupanua barabara.
“Hata ingawa ni muhimu wenye magari kuwa waangalifu, hata serikali iwajibike kwa kuhakikisha barabara ziko sawa,” alisema Onyango.