Huku usajili wa wapiga kura ukiwa karibu kufika ukingoni kote nchini, Mwakilishi wa wadi ya Bogeka eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, Charles Nyagoto amesema zoezi hilo halistahili kuongezewa mda.
Kulingana na Mwakilishi huyo kufanya hivyo ni kutumia vibaya pesa za umma kwani jinsi idadi ya wakaazi wanaojitokeza kwa zoezi hilo hakuna muujiza utatendeka ili waje kwa wingi hata mda ukiongezwa.
Akizungumza nasi siku ya Alhamisi Nyagoto alisema muda wa usajili kutoongezewa kamwe hadi wakati mwingine zoezi hilo litaporejerewa tena.
“Kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanapendekeza mda wa usajili kuongezewa, mimi sikubaliani nao maana wakaazi ambao wamejitokeza ni wachache na hakuna haja ya muda wa usajili kuongezewa,” alisema Charles Nyagoto.
Wakati huo huo, Mwakilishi huyo aliwahimiza wakaazi katika kaunti ya Kisii kuchukua vitambulisho kwa wingi ili kujisajili kama wapiga kura wakati mwingine na kupata fursa ya kuwachagua viongozi ambao watawaleta maendeleo .
“Wale ambao wamefikisha umri wa miaka 18 washike vitambulisho na wakati mwingine usajili wa wapiga kura ukifika wajisajili kama wapiga kura,” aliongeza Nyagoto.