Kiongozi wa chama cha ANC, Bwana Musalia Mudavadi, amewataka inspekta mkuu wa polisi na waziri wa usalama wa ndani kujiuzulu.
Haya yanajiri kufuatia visa vya kudhulumiwa kwa waandanamaji siku ya Jumatatu wakati wa maandamano kushinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC.
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kufanya mkutano na balozi mpya wa Uingereza nchini Kenya, Bwana Nic Hailey, kujadili joto la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa nchini, Mudavadi aliwakashifu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya wafuasi wa Cord wakati wa maandamano hayo.
"Polisi huwa wanafuata maagizo. Waziri anapopeana vitisho kisha visa kama hivi vinashuhudiwa, basi ni sharti aubebe msalaba huo kwa sababu yeye ndiye aliyepeana maagizo hayo,” alisema Mudavadi.
Aliongeza, “Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinet pamoja na Waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery wana mashtaka ya kujibu kwa kutoa maagizo hayo. Wanapaswa kuomba msamaha na kuachishwa au kuacha kazi mara moja,” alisema Mudavadi.
Aidha, alitaka maafisa wa polisi walio husika katika visa hivyo vya dhuluma dhidi ya waandamanaji kuachishwa kazi na kuchukiliwa hatua za kisheria.