Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi akiwahutubia wakaazi wa Likoni. Picha:Musalia Mudavadi/ facebook.com
Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amesema kuwa muungano wa upinzani wa NASA utaheshimu mikataba yote iliyotiwa sahihi nchini.
Akihutubia umma katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa siku ya Jumapili, Mudavadi alisema kuwa NASA haitakua kama Jubilee ambayo imekiuka mikataba ya madaktari na kusababisha mgomo wa wauguzi hao.
“NASA itahakikisha haikiuki mikataba iliyotiwa sahihi na serikali zilizopita,” alisema Mudavadi.
Aidha, alisema kuwa serikali ya NASA itahakikisha inatimiza matwakwa ya wananchi na wafanyikazi wa umma ili kuepuka migomo ya mara kwa mara.
Mudavadi pia alichukua fursa hiyo kujipigia debe na kutaka kuteuliwa kupeperusha bendera ya muungano huo wa upinzani.