Shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri linapanga kutoa hamasa kwa wakaazi wa Pwani kuhusu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Hassan Abdille, alisema kuwa wanalenga kuwahamasisha wakaazi wa Pwani kuchukua kura kwa wingi ili waweze kushiriki uchaguzi ujao kikamilifu.
Abdille alisema kuwa wakaazi wa Pwani mara nyingi hukosa kujisajili kama wapiga kura jambo ambalo linawafungia kushiriki uchaguzi, na kuwapelekea kushinda wakiulalamikia uongozi mbovu na huduma duni.
“Njia ya pekee itakayo wawezesha Wapwani kupata viongozi bora ni kubiga kura, na ili kushiriki upigaji kura, lazima ujisajili kama mpiga kura,” alisema Abdille.
Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu aidha aliwaonya wakaazi kutowachagua viongozi kwa msingi wa chama wala kikabila, na kuwahimiza kuangazia uwajibikaji na uadilifu.
Hatua ya Muhuri inajiri wakati tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, ikiwa tayari imepanga kuanzisha shughuli ya kuwasajili wapiga kura kuanzia mwezi ujao wa Februari.