Shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri limeandaa warsha ya kuwaelimisha askari wa kaunti jinsi ya kutoa huduma bila kuwanyanyasa wananchi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hatua hii inajiri baada ya wakaazi wa Mombasa kulalamika kuwa wanahangaishwa na a askari hao.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo siku ya Jumatano, afisa mratibu katika shirika hilo Peter Shambi, alisema lengo lao ni kubadili mienendo ya askari hao.

“Zoezi hili linalenga kutoa mafunzo maalum kwa askari hawa kwa sababu tumepokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wananchi kuhusu vile wanavyoendesha shughuli zao,” alisema Shambi.

Wakati huo huo, Shambi aliongeza kuwa maeneo waliyopokea malalamishi mengi zaidi ni Kisauni na Bamburi.

“Tumepokea ripoti kuhusu visa vingi katika maeneo ya Bamburi na Kisauni, ambapo askari hawa wanadaiwa kutumia nguvu kupita kiasi wanapoendesha shughuli za kuweka usalama,” aliongeza Shambi.

Aidha, afisa huyo alidokeza kuwa zoezi hilo litaendelea katika kaunti zinginekatika ukanda wa Pwani ikiwemo Kwale na Taita Taveta.