Serikali kuu imetakiwa kusitisha visa vya mauaji ya kiholela vinavyokisiwa kutekelezwa na baadhi ya maafisa wa polisi nchini.
Mwenyekiti wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI, Khelef Khalifa, amemtaka Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuingilia kati swala hilo na kusitisha visa vya watu kuuawa kiholela na kupotea kwa njia tatanishi hususan katika eneo la Pwani.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumanne baada ya hafla ya kukumbuka watu waliopotea katika hali ya kutatanisha, Khalifa alisema kuwa zaidi ya watu 70 eneo la Pwani wamepotea katika hali isiyofahamika.
"Ripoti tuliyokusanya imeonyesha zaidi ya watu 70 wameangamizwa katika hali ya kutatanisha na wengine kupotea mikononi mwa maafisa wa polisi. Hilo sisi hatutakubaliana nalo na lazima serikali isitishe visa hivyo,” alisema Khelef.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa Shirika la Haki Yetu, Padri Gabriel Dollan, amesema kuwa serikali ina jukumu la kulinda wananchi na wala sio kuwaua kiholela.
Alisema kuwa hatua hiyo imewafanya Wakenya wengi kuhisi kutokuwa na imani na maafisa wa polisi.
Wanaharakati hao wamesisitiza kusitishwa kwa visa hivyo na kupendekeza mtu yeyote atakayepatikana na hatia kufikishwa mahakamani badala ya kupotea mikononi mwa maafisa wa polisi.