Mashirika ya kijamii katika eneo la Pwani yameilaumu serikali ya Jubilee kwa kuyakandamiza.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI, Hassan Abdille, ameutaja uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta kama uliosheheni visa vya kukandamiza mashirika hayo.
“Mashirika ya kutetea haki za binadamu hayapewi nafasi kutekeleza kazi yake kwa mujibu wa katiba,” alisema Abdi.
Abdille alisema kuwa ukandamizaji huo umechagia kugawanyika kwa mashirika hayo na kuweka taswira ya mashirika yanayounga mkono serikali na yale yanayoipinga.
Akizungumza katika warsha iliyowaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili hali ya usalama na ukiukaji wa haki za binadamu katika Kaunti ya Mombasa, Abdille alisema iwapo serikali itatoa nafsi pasi kuyakandamiza mashirika hayo, basi nchi hii itakuwa salama zaidi.
Katika warsha hiyo, viongozi mbali mbali walionekana kunyoosha kidole cha lawama kwa vyombo vya usalama kwa madai ya kutoshirikiana vyema na wananchi katika juhudi za kukabili visa vya utovu wa usalama.