Shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI limeitaka mamlaka inayochunguza utendakazi wa maafisa wa polisi IPOA, kuchunguza mauaji ya dereva wa tuktuk aliyepigwa risasi na maafisa wa polisi huko Tiwi.
Tsuma Jeff Mumbo, alipigwa risasi na polisi walipokuwa wakiwafukuza majambazi.
Shirika hilo lilisema kuwa mauaji hayo ni miongoni mwa mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na maafisa wa polisi, na kutaka afisa aliyehusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Athman Mwangoka kutoka shirika hilo amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona afisa wa polisi wa cheo cha juu wakitekeleza mauaji kiholela.
“Hii ni ishara wazi ya utepetevu wa utumiaji wa silaha unaoshuhudiwa miongoni mwa maafisa wa polisi,” alisema Mwangoka.
Alisema kuwa kama shirika watasimama kidete na familia ya mhudumu huyo wa tuktuk ili kuhakikisha haki inatendeka na afisa aliyehusika anachukuliwa hatua za kisheria.
Paul Hesabu, msemaji wa familia ya mhudumu huyo ameitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio hilo pamoja na kufidia familia hiyo.
Wakaazi wa eneo hilo walifanya maandamano na kufunga barabara kwa siku mbili mtawalia kupinga mauaji hayo.