Muungano wa Cord umetakiwa kumpa kiongozi wao Raila Odinga nafasi nyingine ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Wakati uo huo, imejitokeza katika mdahalo wa Jumatano jioni wiki hii kwamba yeyote atakayepewa nafasi ya kupeperusha bendera ya muungano huo katika kinyanganyiro cha urais, kulingana na mkataba wa maelewano wa Cord, atahitajika kuwania mara moja na ashindapo, ataongoza tu kwa hatamu moja na kupokeza, jambo ambalo lilikataliwa mbali na mchanganuzi mmoja mashuhuri wa siasa.
"Katika harakati za kuleta uwiano katika muungano wetu, imepangwa kwamba yeyote atakayeidhishwa kuwakilisha Cord kuwania urais aidha kutoka Chama cha Ford Kenya, Wiper au ODM, atafanya hivyo tu mara moja na akiwa rais, ataongoza tu kwa hatamu moja ili wanaCord wengine pia wapate nafasi," alisema katibu mkuu wa chama cha Wiper ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Mombasa, Hassan Omar.
Hata hivyo, ufichuzi huo wa Bw Omar ulitiliwa shaka na mchanganuzi wa siasa Barack Muluka ambaye alisema itakuwa historia iwapo muwaniaji yeyote wa urais katika muungano wa Cord atafuata kikamilifu matakwa ya mkataba wao wa maelewano.
"Hadi sasa, hakuna kiongozi yeyote wa kisiasa nchini ambaye anaweza kuaminiwa kuenenda kulingana na makubaliano wa chama, tangu enzi za rais mstaafu Mwai Kibaki," alisema.
"Lakini kwa wawaniaji watarajiwa katika muungano huo, ninapendekezea Wakenya Bw Raila Odinga kwa sababu ndiye bado anaweza kupata kura nyingi na hata pengine kushinda urais," alisema Bw Muluka alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini.
"Mchango wa Raila katika mstakabali wa mambo ya taifa hili si wa kusahaulika virahisi ambapo italazimu anyimwe nafasi nyingine na yeyote yule hasa ya kuwania urais kwa niaba ya Cord kama atataka.
Kwa kifupi, hata wanaCord wenyewe waache kumpiga vita na wampe nafasi ya kutosha katika maazimio yake ya kuiongoza Kenya kama urais," alielezea Muluka.