Mbunge wa Kilifi kaskazini amewataka viongozi wanaoshinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya mipaka na uchaguzi kujiuzulu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia umma mjini Kilifi, Gideon Mung'aro alisema kuwa viongozi wanaotaka kuwabandua makamishna wa IEBC wanaonyesha ishara kuwa hawakuchaguliwa kwa njia ya halali, hivyo basi wajivue majukumu kabla ya kuandamana dhidi ya tume hiyo.

“Wale wanaosema kuwa IEBC haifai kwanza wajiuzulu kwa sababu wanapoandamana dhidi ya tume iliyowatangaza washindi, inaashiria kuwa hawakuchaguliwa kwa njia ya halali,” alisema Mung’aro.

Wakati huo huo, mbunge huyo alisema kuwa maandamano hayo huenda yakawa na athari kubwa kwa sekta ya utalii katika kanda ya Pwani.

Aidha, amewataka wazazi na vijana kutotumiwa na wanasiasa wanaotaka kujifaidisha wenyewe.

“Lazima tukubaliane kuwa hali hii ya watoto wetu kupelekwa katika maandamano na kisha kurushiwa vitoa machozi yafaa kusitishwa. Wacheni wafanye maandamano hayo huko Nairobi. Wakaazi wa Pwani wakijuhusisha katika maandamano haya tutaathiri sekta ya utalii,” alisema Mung'aro.

Kaunti ya Mombasa ilishiriki maandamano hayo siku ya Jumatatu kwa mara ya kwanza, huku Spika Thadius Rajwayi akitiwa mbaroni.