Wabunge walioasi mrengo wa Cord wameandaa uchaguzi wao na kumteua Gideon Mung’aro kuwa mwenyekiti wa muungano wa wabunge wa Pwani.
Haya yanajiri miezi kadhaa baada ya wabunge wa Pwani kumteua Gunga Mwinga kama mwenyekiti wa muungano huo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Mbunge wa Lunga Lunga, Khatib Mwashetani, aliyechaguliwa kama msemaji mpy wa muungano huo, alisema kuwa wanamtambua Mung’aro kama mwenyekiti wa muungano huo.
Naibu mwenyekiti mpya wa muungano huo Zeinab Chidzuga, amewataka Wapwani kuunga mkono agenda walizonazo ili kuhakikisha kuwa eneo la Pwani linashirikiana na serikali kuu katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Sisi tumechaguana kwa msingi wa kuzingatia sheria za chama na muungano huu. Wale wanaodai kuwa Mung’aro hafai basi sisi tunawaambia kuwa yeye ndiye mwenyekiti na anatambulika kila mahali,” alisema Chidzuga.
Miezi kadhaa iliyopita, muungano huo ulifanya kikao na kumchagua mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga kama mwenyekiti.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulipingwa vikali na kundi linalongozwa na Mung’aro.
Kwa sasa kuna miungano miwili inayodai kuwawakilisha Wapwani katika maswala mbali ya maendeleo, usalama na ukuzaji wa uchumi.