Mbunge wa Kilifi Kazkazini Gideon Mung’aro amesema kuwa mrengo wa Cord kamwe hautashinda uchaguzi mkuu ujao kufuatia idadi kubwa ya wakenya kutounga mkono mrengo huo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mung’aro amesema kuwa kuendelea kuonyeshana ubabe wa kisiasa baina ya serikali na Cord huenda wakazi wakakosa imani zaidi na mrengo huo kwani umeshindwa kuwaunganisha wakenya na kuwa katika mstari wa mbele kueneza uchochezi na siasa za ukabila.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mung’aro, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Muungano wa wabunge wa Pwani amesema kuwa jinsi viongozi wa mrengo huo wanavyoendelea kumkosoa kwa kuuasi mrengo wa Cord kunaonyesha wazi kuwa siasa zao zimepitwa na wakati na kamwe hawatashinda uchaguzi mkuu ujao.

Amewataka viongozi wa upinzani kutii sheria za nchini iwapo wanatetea demokrasia kama wanavyosema katika mikutano ya kisiasa, na akawahimiza wananchi kutokubali kulaghaiwa na baadhi ya viongozi walafi wanaodai kuwa wanapigania haki zao kumbe wana malengo fiche.

“Tafadhali wananchi jiepusheni na baadhi ya hawa viongozi wanaodai kuwa wanawatetea, lakini ukweli mtupu wana malengo yao binafsi hasa mrengo wa Cord hauna mwelekeo wowote, ndio maana watashindwa katika uchaguzi mkuu na serikali ya Jubilee,” alisema Mung’aro.

Kiongozi huyo hata hivyo ameshtumu hatua ya Cord kwa kukosoa Tume ya IEBC kwa madai kuwa inaegemea upande Jubilee, kufuatia jinsi ilivyotupilia mbali saini walizokusanya.