Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro amesema kuwa gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho anafaa kutii sheria za nchini jinsi inavyohitajika ili kuzuia kushuhudiwa kwa mgogoro.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mung’aro amesema kuwa kuendelea kuonyeshana ubabe wa kisiasa baina ya gavana huyo na serikali huenda wakaazi ndio wanaumia zaidi kutokana na jinsi serikali ina uwezo wa kukatisha shughuli zote muhimu kwa kaunti hiyo.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Mung’aro ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa muungano wa wabunge wa Pwani amesema kuwa jinsi viongozi wanavyomuunga mkono kukiuka sheria za nchini ndivyo wanavyochangia masaibu zaidi nchini.

Amewataka viongozi wa upinzani pamoja na gavana Joho kutii sheria za nchini iwapo wanatetea demokrasia kama jinsi wanavyosema katika mikutano ya kisiasa na akawahimiza wananchi kutokubali kulaghaiwa na baadhi ya viongozi walafi wanaodai kuwa wanapigania haki zao kumbe wana malengo fiche.

“Tafadhali wananchi jiepusheni na baadhi ya hawa viongozi wanaodai kuwa wanawatetea lakini ukweli mtupu wana malengo yao binafsi kwa sababu kama hao wanatetea demokrasia basi sio sababu ya kiongozi kukaidi kutii sheria,” alisema Mung’aro.

Kiongozi huyo hata hivyo ameshtumu uchaguzi wa hivi majuzi wa viongozi wa Pwani akisema kuwa ulikuwa uchaguzi wa kibinafsi ili kuondoa viongozi waliyotangaza kushirikiana na serikali licha ya kuwa katika mrengo wa Cord.