Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro ameyapinga matamshi ya gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho kuwa mkoa wa Pwani ni ngome ya mrengo wa Cord.
Mung’aro ambaye ni mmoja wa wabunge waasi wa chama cha ODM, amesema kuwa Wapwani tayari wamegutuka kutoka usingizini na kuwa hawatakubali kushurutishwa kumpigia mtu kura kwa msingi wa chama ila kulingana na utendakazi wake.
"Mtu asikudanganye kwamba Pwani ni ngome ya Cord, hiyo hakuna na haitawahi kuwa tena. Tumekwisha kata kauli na haturudi nyuma kamwe," alisema Mung’aro.
Mbunge huyo vilevile amewataka wakazi wa Pwani kuwachagua viongozi wenye maono ili kuhakikisha kuwa wanafaidika kimaendeleo badala ya kusalia nyuma wakati maeneo mengine yakizidi kujiendeleza.
Mung’aro pia amesisitiza kuwa atakipigia debe chama kipya cha JAP kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi ujao kwani ana imani kuwa chama hicho ndicho chenye uwezo wa kutatua shida za Pwani.
Mbunge huyo alikuwa akizungumza mjini Malindi siku ya Jumanne alipoongoza kampeni za kumpigia debe mwaniaji wa kiti cha ubunge wa Malindi kwa tiketi ya chama cha Jubilee.
Kauli yake inaonekana kumjibu gavana Joho ambaye alinukuliwa siku ya Jumamosi iliyopita akisema kuwa Pwani ni ngome ya Cord na kwamba muungano huo utazidi kuupata uungwaji mkono katika eneo hilo.