Kijana mwenye umri wa makamo amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kudai kuwa alitumwa na Mungu kujirusha baharini katika kivuko cha Likoni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Benson Mwigai, anadaiwa kujaribu kujitoa uhai kwa kujirusha katika kivuko cha Likoni mnamo Mei 31, mwaka huu.

Iliwalazimu wavuvi kumuokoa jamaa huyo na kumpeleka kwa maafisa wa usalama katika kituo cha polisi cha feri.

Mwigai alikubali shtaka hilo siku ya Jumanne, na kuieleza mahakama kuwa alikuwa ametoka Kiambu na alikuwa ametumwa na Mungu wake kuja kujirusha majini.

“Mungu alinituma nije nijirushe katika kivuko cha Likoni, sasa sikuwa na budi ila kutekeleza amri hiyo,” alisema Mwigai.

Kauli yake iliufanya upande wa mashtaka kuomba muda wa mwezi moja ili aweze kufanyiwa uchunguzi wa akili.

Hakimu Lilian Lewa alikubali ombi hilo na kuagiza kesi hiyo kutajwa Agosti 24, mwaka huu.