Mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya katika Kaunti ya Kisii ambaye pia ni mlezi wa kidini katika Chuo Kikuu cha Kisii Kasisi Lawrence Nyaanga ameomba mashirika ya kutoa mikopo kwa vikundi vya akina mama kuchunguza ni biashara ipi pesa hizo zitafanya.
Hii ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya vikundi vya akina mama hukopa pesa kutoka mashirika hayo kisha baadaye hutumia pesa hizo kupika pombe haramu ambayo ni kinyume na sheria.
Akizungumza nasi mjini Kisii Nyaanga alisema wakati shughuli ya kumwaga pombe hufanywa katika vijiji mbalimbali baadhi ya wagema hujuta watatoa pesa wapi ili kurudisha mikopo waliyokopa katika mashirika hayo.
“Tumegundua kuwa kuna wagema ambao hukopa pesa kupitia vikundi kisha wanatumia pesa hizo kupika pombe haramu ambayo ni kinyume na sheria,” alisema Nyaanga.
“Ninaomba mashirika yote ya kutoa mikopo kufanya uchunguzi kwa pesa wanazotoa kwa vikundi vya akina mama," aliongeza Nyaanga.
Aidha, Nyaanga aliwaonya wagema wanaoendelea kufanya biashara hiyo huku akiomba wakaazi kufikisha habari wanaposhuhudia upishi wa pombe haramu ili wagema hao wachukuliwe hatua kali za kisheria.